Exodus 10:20-27

20 aLakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke.

Pigo La Tisa: Giza

21 bKisha Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili giza litande katika nchi ya Misri, giza ambalo watu wanaweza kulipapasa na kulihisi.” 22 cKwa hiyo Mose akaunyoosha mkono wake kuelekea angani, na giza nene likafunika pote katika nchi ya Misri kwa muda wa siku tatu. 23 dHakuna mtu yeyote aliyeweza kumwona mwenzake, wala kuondoka mahali alipokuwa kwa muda wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga katika maeneo yao waliyokuwa wanaishi.

24 eNdipo Farao akamwita Mose na kusema, “Nendeni, mkamwabudu Bwana. Hata wanawake na watoto wenu mwaweza kwenda nao pia, lakini kondoo, mbuzi na ngʼombe wenu waacheni.”

25 fLakini Mose akasema, “Huna budi kuturuhusu tuwe na dhabihu na sadaka za kuteketezwa za kutoa mbele za Bwana Mungu wetu. 26Sisi ni lazima tuondoke na mifugo yetu pia, wala hakuna ukwato utakaoachwa nyuma. Inatupasa kutumia baadhi ya hiyo mifugo katika kumwabudu Bwana Mungu wetu, kwa kuwa mpaka tutakapofika huko hatutakuwa tumefahamu ni nini tutakachotumia katika kumwabudu Bwana.”

27 gLakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, hakuwa radhi kuwaachia waondoke.
Copyright information for SwhNEN